Katibu Mkuu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa,alisema Magufuli hawezi kushindana na Ukawa, kwani kwenye jimbo lake la Chato chama hicho kimechukua sehemu kubwa ya uongozi kuanzia ngazi ya mitaa na kata.
Dk. Slaa alisema ikiwa kwenye jimbo lake mwenyewe Ukawa wamempita kwa nafasi hizo, hatakuwa na uwezo wa kushindana nao katika nafasi hiyo ya juu kabisa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alipongeza mchakato wa mchujo uliofanywa na CCM katika kumpata mgombea.
Hata hivyo alisema Magufuli anahitaji msaada wa kidiplomasia kwani utendaji wa mtu akiwa Waziri ni tofauti na wakati akiwa Rais.
“Walikuwa na mchakato mgumu kidogo hasa walipofikia kundi la watano, napongeza walipofikia. Huyo mgombea waliyempata, Watanzania wanamfahamu, ni mchapakazi…lakini utendaji wa mtu akiwa Waziri ni tofauti na akiwa Rais…anahitaji msaada wa kidiplomasia,” Dk. Bisimba.
Mhadhiri mwandamizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Dk. Benson Bana, alisema CCM hawajafanya makosa kumteua Magufuli kuwapeperushia bendera kwani ni mtu ambaye hajitambulishi kimakundi huku akijipatia umaarufu katika utendaji na uchapaji wake wa kazi katika wizara ikiwamo ya Ujenzi.
Alisema, Magufuli ni mtu ambaye anafaa kukiwakilisha CCM kupambana na vyama vya upinzani kwani akiwa Waziri, wizara yake haina historia yoyote ya kashfa katika taarifa za Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salim, aliipongeza CCM kwa kufanikiwa kuvunja makundi yaliyokuwa yametawala kabla ya kupatikana kwa mgombea huyo.
Alisema CCM kumpitisha Dk. Magufuli kumevunja makundi yote yaliyokuwamo, jambo ambalo halikutarajiwa.


0 Response to "SLAA: MAGUFULI Hawezi Kushindana na UKAWA, Jimboni Kwake Tu Kachemka!"
Post a Comment