Wafanyakazi wa kiwanda cha mikate cha Grand Confectionery Bakery cha Keko jijini Dar wakiwa ‘wamemtaiti’ Bosi wao, Yahya.
Brighton Masalu
‘TUGEE chetu’! Ndiyo kauli iliyotolewa na wafanyakazi wa kiwanda cha mikate cha Grand Confectionery Bakery cha Keko jijini Dar, baada ya ‘kumtaiti’ bosi wa kiwanda hicho aliyejulikana kwa jina moja la Yahya mwenye asili ya India kwa kumfungia ndani huku wakimkaba kwa zaidi ya takriban saa 12 wakishinikiza kulipwa haki ya mafao yao.
Sekeseke hilo lilijiri Jumatano iliyopita ambapo kikwazo kilichosababisha mzozo huo kukolea, ni kitendo cha bosi huyo kuwalazimisha wafanyakazi hao kusaini barua ya kusimamishwa kazi kutokana na kile alichokiita kiwanda kufungwa kwa muda bila kuwalipa mafao yao.
Awali, akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu mmoja wa wafanyakazi hao alisema, kilichoongeza hasira zaidi ni kitendo cha mwajiri wao huyo kugoma kuwalipa mshahara wa mwezi uliopita (Juni) hadi wasaini barua hiyo ya kuachishwa kazi bila kupewa mafao.
“Kilichotukasirisha zaidi ni kitendo chake cha kugoma kutulipa hata mshahara wa mwezi wa sita, eti hadi tusaini barua ya kuachishwa kazi bila malipo ya mafao yetu akidai atatuita siku nyingine ya kutupa mafao.
“Sisi tunataka tusaini siku atakayotulipa mafao yetu lakini mshahara atupe, lakini imekuwa ni kawaida yake kila ukifika mwisho wa mwezi wakati wa kutoa mishahara kuwa na visa vingi,” alisema mfanyakazi huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Mwandishi wetu alifika eneo la tukio na kushuhudia sakata hilo ambapo katika mazungumzo yake na mwajiri huyo, alisema anawataka wasaini barua za kuachishwa kazi na kuwalipa siku nyingine la sivyo hakuwa tayari kuwalipa hata mishahara jambo lililopingwa vikali na upande wa pili.
“Wanafanya fujo bila kusikiliza vizuri maelekezo yangu, wametufungia ndani tangu asubuhi hadi sasa (saa 1:30 usiku), tumefunga na hatujala na mbaya zaidi wamejaribu hata kunipiga, hii ni haki na sheria kweli?,” alisema Yahya mbele ya mwandishi wetu.
Hata hivyo, baadaye waliitwa polisi na walipofika kwa kutumia busara na weledi wa kisheria, walifanikiwa kutatua sakata hilo kwa mwajiri huyo kuwalipa mishahara wafanyakazi hao na kuwatangazia siku ya kusaini barua ya kuachishwa kazi pamoja na kuwalipa mafao yao, zoezi ambalo lilitekelezwa na ‘mdosi’ huyo chini ya usimamizi wa askari polisi.
Hadi gazeti hili ‘linaanua matanga’ kutoka eneo la tukio, wafanyakazi hao walikuwa wakitangaziwa kurudi Julai 13, mwaka huu kwa ajili ya malipo ya mafao yao na kusaini barua ya kuachishwa kazi kutokana na kiwanda kupata hasara.



0 Response to "TIMBWILI ZITO: BOSI MDOSI ALA KIBANO TOKA KWA WAFANYAKAZI WAKE JIJINI DAR -PICHAZ"
Post a Comment