Latest Updates

HII SASA KALI....STRAIKA FORCE

Waandishi Wetu,
Dar es Salaam
UNAWEZA kusema ni ‘straika force’ yaani nguvu ya mashambulizi kwa tafsiri inayoshabihiana na mazingira ya soka la Bongo, kwani Simba na Yanga zote zimeonekana kujiimarisha katika safu za ushambuliaji.
Amissi Tambwe na Simon Msuva wakishangilia kwa pamoja.
Msimu uliopita, Yanga ilitwaa ubingwa huku ikionekana kuwa na safu nzuri ya ushambuliaji kwani ilifunga mabao 52 katika Ligi Kuu Bara huku Simba ikionekana kusuasua na kufunga 38 kwenye ligi hiyo.
Ukitazama usajili wa timu zote mbili, nguvu kubwa imewekwa katika safu zao za ushambuliaji kwani Yanga yenye Amissi Tambwe na Simon Msuva ambaye ni mfungaji bora wa msimu uliopita, imewasajili mastraika Donald Ngoma na Malimi Busungu.
Mshambuliaji wa timu ya Simba, Emmanuel Okwi.
Kwa mujibu wa Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, wameongeza mastraika hao ili kuiongezea nguvu safu yao ya ushambuliaji ambayo ilifanya vizuri msimu uliopita.
“Tunataka tuwe bora zaidi, hatujali kama nyuma tulifanya vizuri kwani adui anaweza kuja kivingine,” alisema Pluijm, raia wa Uholanzi.
Mshambuliaji wa timu ya Simba, Hamis Kiiza enzi akiwa Yanga.
Simba nayo ambayo msimu uliopita ilifunga mabao 38 huku nyota wake Emmanuel Okwi akifunga mabao kumi kati ya hayo, nayo imeimarisha nguvu kikosini kwa kuwasajili mastraika Laudit Mavugo, Hamis Kiiza na Mussa Mgosi.
Mavugo anatokea Vital’O ya Burundi, Kiiza aliichezea Yanga katika mzunguko wa kwanza msimu uliopita na Mgosi amemaliza mkataba wake Mtibwa Sugar.
Kocha wa Simba Dylan Kerr, ambaye timu yake itaingia kambini katikati ya wiki ijayo huko Lushoto mkoani Tanga, atahakikisha timu yake itacheza soka la kasi na la kushambulia muda wote ili wapate mabao mengi.
“Nimetazama rekodi za msimu uliopita na kuona timu haikuweza kufunga mabao mengi, nitatumia mifumo kama minne hivi ili kuifanya timu iweze kufunga mabao mengi,” alisema Kerr, raia wa Uingereza.

MSUVA, NGOMA WAFUNGA MABAO 37
Kwa upande wa Yanga, hata kama ukiachana na Tambwe, Msuva msimu uliopita aliifungia timu yake jumla ya mabao 21 ambapo 17 alifunga katika ligi kuu na manne kwenye Kombe la Mapinduzi wakati Ngoma anayetokea FC Platinum ya Zimbabwe, aliifungia timu yake mabao 16 msimu uliopita, 10 katika ligi kuu na sita katika michuano mingine, hivyo wawili hao wamefunga mabao 36 ikiwa ni pungufu ya mawili waliyofunga Simba msimu uliopita katika ligi kuu.
Hata hivyo, Yanga bado ina wafumania nyavu wengine ambao ni Tambwe aliyefunga mabao 17 msimu uliopita (14 kwenye ligi, matatu Kombe la Shirikisho Afrika) na Busungu aliyeifungia Mgambo JKT mabao tisa. Pia Yanga yupo kiraka Joseph Zutta aliyefunga mabao manne akiichezea Medeama SC ya Ghana msimu uliopita.

OKWI, KIIZA WATISHIA AMANI
Usikidharau hata kidogo kikosi cha Simba, kwani uwezo wa washambuliaji wake, Mavugo, Okwi, Kiiza na Mgosi unatishia amani kwani wote wana uwezo mkubwa wa kufunga.
Mavugo akiwa na Vital’O ya Burundi, msimu uliopita alifunga mabao 34 huku Okwi akiifungia Simba mabao kumi, Kiiza alifunga mabao 12 akiwa na Yanga msimu wa 2013/14 na Mgosi akiwa Mtibwa msimu uliopita alifunga mabao matano.

KAZI IPO KWA KERR, PLUIJM
Licha ya vikosi hivyo kuonekana vipo imara, kazi kubwa inabaki kwa makocha Kerr na Pluijm kwani wanatakiwa kuunda muunganiko mpya wa mastraika wao, pia safu za ulinzi.
Katika ulinzi msimu uliopita, Yanga ilifungwa mabao 18 wakati Simba ilipigwa mabao 19 katika ligi kuu, hii inamaanisha katika ulinzi timu hizo hazijatofautiana sana.
Kazi kubwa ya makocha hao itakuwa kuimarisha muunganiko wa viungo na washambuliaji ili kuweza kupata mabao mengi zaidi uwanjani.
Kerr alisema anaweza kutumia mfumo wa 4- 4- 2, 4-3-3, 4-5-1 au 4-4-1-1, kutegemea nguvu anayokutana nayo. “Naweza kuanza na 4-4-2, nikiona haunipi faida nawawekea 4-3-3 hadi huo wa mwisho lazima tupate bao,” alisema Kerr.
Kwa upande wake, Pluijm alisema: “Mimi napenda kutumia 4-4-2 au 4-5-1 huku mawinga wakifanya kazi zaidi na mambo yakienda hovyo naweza kupita katikati na siyo pembeni.
“Mashambulizi yangu yatategemea na nguvu ya kuzuia ya wapinzani wetu uwanjani, si unajua timu huja tofauti.”  Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana katika msimu ujao wa ligi kuu.
Wilbert Molandi, Shaaban Mbegu na Sweetbert Lukonge.

0 Response to "HII SASA KALI....STRAIKA FORCE"

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...